Higher Education Students' Loans Board
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imefanya mbio za hisani leo Februari 15, 2025 katika viwanja vya Farasi vilivyopo Oysterbay Jijini Dar es salaam kama sehemu ya maadhimisho ya miaka ishirini tangu kuanzishwa kwa HESLB.
Lengo la mbio hizo za hisani ni kuimarisha afya, kukusanya fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya maabara kwa ajili ya shule mbili za sekondari (moja ni ya Zanzibar na nyingine ni ya Tanzania bara) na kuboresha kituo cha huduma kwa wateja cha HESLB.
Akizungumza katika hotuba yake kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwakilishi wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Uwakilishi Zanzibar Mhe. Hamza Hassan Jumaa ameipongeza Bodi ya Mikopo kwa mafanikio makubwa katika kuwezesha vijana wengi wa kitanzania kupata elimu ya juu na kuandaa nguvu kazi ya taifa lenye wataalamu wa fani mbalimbali hapa nchini.
“Serikali kupitia Bodi ya Mikopo, imewezesha vijana takribani laki nane (800,000) kupata elimu ya juu…hivyo basi maadhimisho haya ya miongo miwili ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ni fursa ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana na kujipanga kwa ajili ya mafanikio makubwa zaidi katika siku zijazo’’, amesema waziri Jumaa.
Aidha, amemshauri Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kuendelea kuweka mikakati ya kuongeza vyuo na kampasi za vyuo vikuu vingi kule Zanzibar vitakavyokidhi mahitaji ya vijana ili kuendelea kuimarisha udugu katika nyanja zote za kijamii, kisiasa na kiuchumi kupitia uwezeshaji katika elimu ya juu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. QS Omary Kipanga amesema kuwa mwaka 2021/22 wakati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaingia madarakani bajeti ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ilikuwa shilingi bilioni 464, ambapo ndani ya miaka minne ya uongozi wake, bajeti imepanda hadi kufikia shilingi bilioni 787.
“Kwa kipekee Mheshimiwa mgeni rasmi, tufikishie shukrani zetu kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Dkt. Hussein Mwinyi kwa kazi hii kubwa ya kupandisha bajeti ya Bodi ya Mikopo kwa zaidi ya asilimia 90. Sisi kama Wizara tunajivunia na tunashukuru viongozi wetu kwa utashi wao wa kuona eneo hili la elimu ni eneo muhimu sana”, amesema Mhe. Kipanga.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia amesema kuwa Bodi hiyo ilipoanzishwa mwaka 2004 ilianza na wanafunzi elfu arobaini na nane tu (48,000) ikiwa na bajeti ya shilingi bilioni 53.1 na kwamba kadri miaka ilivyokuwa ikisonga mbele ndivyo kiasi cha fedha kilivyokua kikiongezeka.
“Kwa mwaka 2024/2025, shilingi bilioni 787 zimetolewa kwa ajili ya wanafunzi laki mbili na elfu arobaini na tano, mia saba tisini na tisa (245,799), ambapo jumla ya mikopo iliyotolewa na Bodi tangu kuanzishwa kwake ni kiasi cha shilingi trilioni 8.2 ambacho kimeweza kusomesha wanafunzi laki nane na elfu thelathini (830,000) nchi nzima” amesema Dkt. Kiwia.
Maadhimisho ya miaka 20 ya HESLB yenye kauli mbiu inayosema, “Miongo Miwili ya Athari Chanya, Ubunifu na Huduma”, yaliyoanza tangu tarehe 10 Februari, 2025 kwenye maeneo mbalimbali nchini, yatafikia kilele chake Februari 17, 2025 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es salaam.